Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza vitendo vilivyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili nchini, imeanza rasmi kazi kwa kupokea taarifa na malalamiko mbalimbali kuhusu operesheni hiyo.
Aidha, katika kufanikisha majukumu yake, Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji na Balozi mstaafu Hamisi Msumi, itatembelea maeneo mbalimbali nchini ili kukutana na wananchi wenye taarifa au malalamiko kuhusiana na jinsi Operesheni Tokomeza ilivyofanyika.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Tume hiyo, Frederick Manyanda katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, jana.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, taarifa au malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa operesheni hiyo yatapokelewa kwa njia mbalimbali, zikiwemo kwa posta, baruapepe na hata simu za mkononi.
Amezitaja namba zitakazotumika kuwa ni 0714 826 826, 0767 826 826, 0787 826 8265 na 0773 826 826. Aidha, baruapepe ni opereshenitokomeza@agctz.go.tz na kwa watakaopenda kutoa taarifa au malalamiko kwa njia ya barua, watalazimika kupitishia barua zao kwa Katibu wa Tume, Tume ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili, S.L.P 9050, Dar es Salaam.
Tume hiyo iliundwa na kutangazwa Mei 2 mwaka huu na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue kuwa, Rais ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32.
Hatua ya Rais Kikwete kuunda tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi, Sura ya 32 ilikuja baada ya Operesheni Tokomeza Ujangili kusitishwa na Bunge kutokana ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.
Operesheni hiyo iliyoanza Oktoba mwaka 2013 na kusitishwa Novemba 4 mwaka jana, ndiyo iliyowang’oa mawaziri wanne kwa kile kilichodaiwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wake.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Wakati wa kutangaza tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliyataja majukumu ya tume hiyo kuwa ni pamoja na kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa.
Majukumu mengine ni kuchunguza na kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza Operesheni Tokomeza na kuchunguza na kubaini iwapo yupo mtu yeyote aliyekiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea wakati wa Operesheni Tokomeza.
Kuchunguza na kubaini kama wapo watu wowote waliokiuka Sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki.
Kupendekeza hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea za Operesheni Tokomeza.
Kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.