KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema hajawahi kupokea barua yoyote kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, inayowataka waitishe mkutano wa Kamati Kuu ili kufanya marekebisho ya Katiba yao.
Wakati Dk. Slaa anatoa kauli hiyo, Julai, mwaka huu, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, John Mnyika, alizungumza na vyombo vya habari kuwa Agosti, 2006 walifanya marekebisho makubwa ya Katiba ikiwamo kifungu kilichokuwa kinaweka ukomo wa uongozi.
Juzi, Jaji Mutungi alisema kuwa kinachotokea sasa ndani ya chama hicho ni matokeo ya kupuuzwa ushauri wake wa kukitaka kifanye marekebisho ya Katiba yake.
Kauli za viongozi hao zilitokana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwekewa pingamizi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya uenyekiti taifa, akidai chama chake kimekiuka Katiba na maagizo ya msajili.
Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema ya Januari 15, mwaka huu, ilitaka chama hicho kuitisha mkutano rasmi na halali kwa mujibu wa Katiba yao.
“Chama chenu kiitishe mkutano (forum) rasmi na halali kwa mujibu wa Katiba yenu, kisha mlifanyie upya tafakari stahiki suala linalohusu marekebisho ya ibara 6.3.2(c) kwa kuzingatia taratibu na hatua zinazopaswa ili kuwezesha kuwasilishwa kwa ibara hiyo katika Mkutano Mkuu, kwa lengo la kupitishwa rasmi na mkutano huo ambao ndio wenye mamlaka halali kwa mujibu wa Katiba ya chama chenu, ili kuwezesha kutumika kihalali,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Jana, Dk. Slaa alisema hakuna barua yoyote ndani ya ofisi yake ambayo imetoka kwa msajili huyo.
“Sijawahi kupokea barua ya Jaji Mutungi na wala hakuna barua ya aina hiyo ofisini kwake inayoitaka ofisi yangu kuitisha mkutano wa Kamati Kuu ili kufanya marekebisho ya Katiba ya chama,” alisema Dk. Slaa.
Akizungumzia rufaa ya Mbarouk, Dk. Slaa alieleza kushangazwa kwa kitendo cha kupelekwa kwenye magazeti badala ya kufika kwanza ofisini kwake.
“Kwanza siwezi kuzungumzia rufaa ya Mbarouk kwa sababu kuna taratibu zake… lakini kilichonishangaza ni kitendo cha rufaa kupitia kwanza kwenye magazeti badala ya kuletwa kwanza ofisini,” alisema.
Alipotakiwa kuzungumzia kauli ya msajili kuwa walipuuza ushauri wake, alisema hata habari iliyokuwa imeandikwa haikuwa ya kweli bali jaji huyo alilishwa maneno ambayo hayakusema.
“Bora hata umejileta mwenyewe… nimetoka kuzungumza na Jaji Mutungi amesema maneno yaliyoandikwa katika gazeti lenu hayakuwa yake kabisa.
“Ninajua kwanini mnayaandika na malengo yenu nayajua sasa kama mnafanya propaganda tumieni akili.
“Sasa kaandike hivyo hivyo na usipoandika hayo niliyokueleza ni wazi gazeti lenu litakuwa na nia mbaya na Chadema… ukiwa na swali jingine wewe niulize tu,” alisema Dk. Slaa.
Mwandishi alipomtafuta Jaji Mutungi ili kujua kama ni kweli amemweleza Dk. Slaa kuwa hakuyasema maneno hayo, alisema hawezi kuzungumza kwenye simu na badala yake atafutwe leo.
Chanzo: Mtanzania
Chanzo: Mtanzania