Featured Posts

Sunday, September 21, 2014

CHADEMA WATOA KAULI JUU YA MAANDAMANO BILA KIKOMO

Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimesisitiza kuwapo kwa
maandamano yasiyo na kikomo
yatakayoanza leo katika baadhi ya mikoa
licha ya jeshi la polisi kuzuia.
Chama hicho kimesema maandamano
hayo yana lengo la kushinikiza
kuahirishwa kwa Bunge la Katiba
linaloendelea mjini Dodoma.
Malengo mengine ni kuitaka Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba itekelezwe katika
upatikanaji wa Katiba mpya na kupinga
uchakachuaji dhidi ya maoni yaliyotolewa
na wananchi kupitia Tume ya Jaji Mstaafu
Joseph Warioba.
Akizungumza na NIPASHE , Mkuu wa
Idara ya Mawasiliano wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Tumaini Makene, alisema tayari mikoa
kadhaa na wenyeviti wa mikoa wa chama
hicho, wameshapeleka barua polisi ili
kutekeleza hilo.
Alisema barua hizo lengo lake ni kupata
ushirikiano wa kiulinzi kwa jeshi hilo na
siyo kuomba kibali kama ilivyozoeleka.
Alisema mikoa ambayo leo itaandamana
ni Iringa, Arusha na Morogoro huku
Tanga, Manyara, Kilimanjaro, Mbeya,
Mwanza na Musoma wanatarajia
kuyafanya Jumatatu.
ARUSHA WAJIANDAA NA MAANDAMANO
Chadema mkoa wa Arusha, kimesema
maandamano yatakayoanza leo
waandamanaji watavaa vitambaa vyeupe
kusisitiza amani.
Akizungumza jana kwa njia ya simu,
Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa
Arusha, Amani Golugwa , alisema
wamepokea barua ya Polisi ambayo
imezuia maandamano na mkutano wa
hadhara waliopanga kufanya leo. Alisema
katika barua hiyo hakuna sababu za
msingi zilizotolewa hivyo Chadema na
Ukawa wataandamana kwa lazima na
hakuna mtu yeyote atakayeguswa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha, Liberatusi Sabasi, alisema hakuna
maandamano yaliyoruhusiwa na
atakayeandamana atakabiliana na mkono
wa sheria.
Wakati hali hiyo ya sintofahamu
ikiendelea baadhi ya makada wa chama
hicho wameonekana wakiwa katika
harakati za kupamba magari yao kwa
maandishi ya kulaani Bunge la katiba
kama maandalizi ya maandamano ya leo.

TUMEAMIA HUKU