Featured Posts

Saturday, June 7, 2014

SOMA HII UTUPE MAONI YAKO: MASKINI YULE MGONJWA ALIYETELEKEZAWA AFARIKI DUNIA,

Dar es Salaam. Mgonjwa wa saratani ambaye alidai kupewa tiba feki za mionzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (OCRI), Pendo Shoo amefariki dunia  juzi wilayani Karatu akiwa safarini kuelekea Kirua Vunjo, Kilimanjaro kwa wazazi wake.
Mdogo wa Pendo, Digna Shoo, alisema dada yake alifariki juzi, saa nne usiku wakati wanafamilia wakimfanya maombi.
“Alianza kubadilika ghafla wakati tukiwa katikati ya maombi, alilegea na mgongo wake ukawa kama unapinda hivi, tukamshika na tukamweka kitandani,” alisema.
 Digna alisema kwamba baada ya kumweka kitandani  mtumishi wa Mungu aliyekuwa nyumbani hapo alimwombea na hazikupita dakika nyingi akakata roho. Alisema Pendo alikwenda Karatu akitokea Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita, kipindi ambacho hali yake ilikuwa imeshatetereka sana kiasi cha kushindwa kutembea mpaka apate msaada wa mtu karibu.
“Wakati tunatoka Dar es Salaam kuja Karatu, hali yake ilikuwa imeshakuwa mbaya, alikuwa hawezi kutembea bila kumpa ‘support’ (msaada) alikuwa anapepesuka,” alisema Digna.
Digna alisema safari ya dada yake haikuwa imelenga kuishia Karatu, bali walikuwa wanaelekea Kirua Vunjo, Kilimanjaro ambako ni nyumbani kwao alipozaliwa, lakini mauti yalimkuta msichana huyo kabla hajafika.
Kwa maelezo ya Digna, Pendo alikuwa amekata tamaa ya kuishi kutokana na saratani hiyo kusambaa katika matiti yake mawili na kumsababishia vidonda vilivyompa maumivu makali.
Itakumbukwa kwamba gazeti hili liliwahi kuripoti mara mbili taarifa kuhusu Pendo; kwanza ni ile iliyohusu mgonjwa huyo kupewa dawa feki ambazo badala ya kumtibu zilimsababishia madhara zaidi na pili ni kuhusu kunyanyapaliwa baada ya taarifa ya awali kuandikwa gazetini.
Pendo alianza kupata tiba OCRI Novemba mwaka jana baada ya kupata rufaa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini katika mchakato wa tiba yake,  alitozwa kiasi cha Sh1.34 milioni na mtumishi wa OCRI, Almasi Matola kinyume na taratibu.
Baada ya gazeti hili kuchapisha habari hiyo, Mei 20 mwaka huu alikwenda katika hospitali hiyo kupata tiba zaidi, lakini alinyanyapaliwa na wahudumu wa OCRI na akielezwa kwamba vipimo alivyochukuliwa awali vilikuwa havionekani.
 “Niliamua kurudi hospitali nikapime tena na nilitoa damu kwa ajili ya vipimo, lakini nilipokwenda tena kuchukua majibu walidai damu yangu imepotea. Kwa hiyo nililazimika kuanza upya, nilitoa damu tena na vipimo vyote vikawa tayari kama X-ray, Ultra sound na nikavipeleka kwa daktari,” alisema Pendo kabla ya kukutwa na mauti.
Alisema alipatwa na hofu zaidi baada ya kwenda kwa daktari wake Dk Dominista Kombe, ambaye alipaswa kumpa matokeo ya vipimo, lakini alishangaa daktari huyo alipomjibu kwamba, “Majibu yako utayajua hukohuko,” akimaanisha kwenye chumba cha tiba ya mionzi. Alisema alipofika chumba cha tiba ya mionzi muuguzi aliyekuwapo alimwambia asubiri kwenye foleni hadi atakapoitwa jina, lakini alikaa zaidi ya saa nzima bila faili lake kuitwa. Alisema baadaye muuguzi alirudi na kumwambia aende nyumbani kwa sababu wagonjwa ni wengi. Lakini wagonjwa wengine waliokuwa kwenye foleni hawakupewa maelekezo hayo na waliendelea kusubiri.
Kutokana na hali hiyo, Pendo aliapa kwamba asingeweza kwenda tena OCRI na badala yake kuamua kusaka tiba asili na kwenda makanisani kwa ajili ya maombi na maombezi. Mara ya mwisho, marehemu aliwasiliana na gazeti hili akiwa safarini kwenda Karatu ambako amefikwa na mauti.

Uongozi wa OCRI
Mkurugenzi wa OCRI , Dk Twalib Ngoma alisema suala la Pendo lilishafanyiwa kazi na  ripoti ya tukio lote ipo kwenye bodi na matokeo ya ripoti hiyo huenda yakatolewa hivi karibuni.
“Mimi nipo likizo...lakini suala hilo lilishafanyiwa kazi kwa sababu hatuwezi kuacha hivihivi lipite bila kuchukua hatua. Tunalifanyia kazi kwa undani kitaasisi,” alisema Dk Ngoma jana kupitia simu yake ya mkononi.
Aliongeza: “Tunajua kuwa gazeti la Mwananchi lilikuwa na nia njema, lakini siwezi kuhukumu na lazima taasisi ifanye uchunguzi.”
 Mkurugenzi wa Tiba wa OCRI, Dk Diwani Msemo alisema uongozi ulichukua hatua za kumpigia simu Pendo na kumwambia arudi hospitali ili akabadilishiwe daktari na dawa, lakini Pendo aliwaambia kwamba yuko Karatu.
“Tulimpigia simu Pendo ili aje atoe na maelezo yake, tusingeweza kuhukumu kwa maelezo ya upande mmoja tu,” alisema Dk Msemo.
Alisema nia ya OCRI ilikuwa ni kusimamia matibabu ya Pendo ikiwemo kumpa tiba akiwa nyumbani kwa sababu taasisi hiyo ina kitengo cha kutoa tiba ya aina hiyo.
Alisema sambamba na hilo, uongozi ulichukua maelezo ya madaktari waliomhudumia Pendo na muuguzi anayedaiwa kupokea fedha na kutoa dawa feki.
Alisema maelezo ya Matola aliyoandika kwa uongozi wa OCRI, ni kuwa dawa aliyompa Pendo ilibakizwa na mgonjwa mwingine ambaye alitaka kurejeshewa fedha zake ndiyo maana alichukua fedha hizo kwa mgonjwa. Hata hivyo, Dk Msemo alisema OCRI haina mamlaka ya kuchukua fedha kwa mgonjwa ili kumpa tiba na badala yake, dawa zilizobaki hutakiwa kurudishwa kwenye kitengo cha dawa.
“Tumewapa barua za maonyo, wengine tumewabadilisha vitengo na hatua zaidi zilikuwa zinaendelea kuchukuliwa lakini mauti yamemkuta kabla,” alisema.

TUMEAMIA HUKU